Waandishi wa Habari Mkoa Wa Singida Watahadharishwa Kuhusu Viashiria vya Rushwa Wakati wa Uchaguzi
Na Mwandishi Wetu,Wajefya Radio – Singida
Waandishi wa habari mkoani Singida wametakiwa kuongeza umakini katika majukumu yao hasa nyakati za uchaguzi, kwa kuvitambua mapema viashiria vya rushwa na kuviarifu wananchi ili jamii ijikinge navyo. Wito huo umetolewa leo katika semina ya mafunzo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ikilenga kuwajengea uwezo wanahabari kuelekea chaguzi zijazo.
Akizungumza katika semina hiyo, Mwezeshaji Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Takukuru mkoa wa Singida, Bwana Benjameni Masyaga, amesema rushwa ya uchaguzi ni moja ya vitendo vinavyohatarisha demokrasia na haki za wananchi. Alisisitiza kuwa waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya jamii na vyombo vya usimamizi wa uchaguzi, hivyo wanapaswa kutumia kalamu zao kulinda uadilifu wa kura ya wananchi.
Kwa mjibu wa Masyaga alivitaja viashiria vitano vinavyoweza kujitokeza nyakati za uchaguzi, ambavyo waandishi wanapaswa kuvifuatilia na kuviripoti kwa ufasaha:
Kugawa fedha au zawadi kwa wapiga kura – Jaribio la kununua kura badala ya kushindana kwa hoja na sera.
Matumizi mabaya ya rasilimali za umma – Kuingiza magari, fedha au majengo ya serikali kwenye kampeni binafsi.
Ahadi za upendeleo binafsi – Kutoa ahadi za ajira, biashara au mikopo kwa lengo la kushawishi kura.
Vitisho kwa wapiga kura – Kuwatisha wapiga kura watakosa ajira au huduma fulani endapo hawatampigia kura mgombea fulani.
Habari za upotoshaji kwenye vyombo vya habari na mitandao – Kutumia taarifa za uongo au propaganda kuchafua wapinzani.
Hata hivyo Bw.Masyaga, Ameongeza kuwa Takukuru hutumia mikakati kadhaa kudhibiti vitendo hivi ikiwemo:
Kutoa elimu ya uadilifu kwa wananchi na vyama vya siasa.
Kufanya ufuatiliaji wa karibu katika maeneo ya kampeni na vituo vya kupigia kura.
Kushirikiana na Jeshi la Polisi ,Tume ya Uchaguzi na Wadau Mbalimbali.
Kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Aisha,Bw.Masyaga alieleza kuwa rushwa ikiachwa, huharibu msingi wa demokrasia na kupelekea kuchaguliwa viongozi kwa misingi ya fedha badala ya sera na uwezo. Matokeo yake ni kushuka kwa imani ya wananchi kwa mchakato wa uchaguzi, kuzorota kwa maendeleo, na kuzuka kwa migawanyiko ya kijamii.
Pamoja na Hayo Zipo Changamoto zinazowakabili Wanahabari katika nafasi yao muhimu kuisaidia Jamii dhidi ya mapambano haya ya Rushwa, Bw.Masyaga alisema bado kuna mianya inayoweza kudhoofisha ufanisi wa waandishi wa habari nyakati za uchaguzi ikiwa ni pamoja na:
Kukosa taarifa za uhakika kuhusu matukio ya rushwa.
Shinikizo kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya habari wenye maslahi ya kisiasa.
Hali ngumu za kiuchumi zinazoweza kuwafanya baadhi ya waandishi kushawishika kwa hongo.
Hofu ya usalama binafsi au ajira kwa kuripoti habari zinazohusu wagombea wenye nguvu.
Upungufu wa mafunzo ya kitaaluma kuhusu sheria na taratibu za uchaguzi.
Akihitimisha, Masyaga aliwaomba waandishi wa habari mkoani Singida kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU, kushikilia maadili ya uandishi, na kuhakikisha wanatoa taarifa kwa usahihi ili kulinda kura na demokrasia ya Tanzania.
Kwa Ujumla Wao,Waandishi Hao Wa Habari Waliahidi Kuitumia Elimu hii Kwa Jamii na Kuhakikisha wanatumia kalamu,na kamera zao Kwa weledi hasa kuwa daraja kati ya Wananchi ,Takukuru na Mamlaka za Serikali hasa nyakati za uchaguzi Kwa kuripoti Kwa Mizania Sawa.
Makala hii endelevu inalenga kuelimisha jamii kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kudhibiti rushwa za uchaguzi. Waandishi wakitimiza wajibu wao, wananchi watapata mwongozo wa kufanya maamuzi kwa uhuru na bila kushawishiwa na fedha au zawadi.